Africarriers yakabidhi basi kwa Simba Queens

Kampuni ya uuzaji wa magari Africarriers imetoa basi kwa timu yetu ya Wanawake ya Simba Queens kwa ajili ya usafiri wa ndani ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya mkataba tuliosaini mwaka jana.

Mkuu wa Rasilimali Watu wa Africarrier, Lydia George amesema baada ya kuona soka la wanaume likiendelea kukua sasa wanaongeza nguvu kwa upande wa wanawake.

Lydia amesema lengo la Africarriers ni kusapoti mpira wa Tanzania kama ilivyo kwa Serikali na Shirikisho la Soka nchini (TFF).

“Tulikubaliana kuwapa mabasi na leo tunakabidhi gari la pili kwa Simba Queens. Mwaka jana tulitoa basi kwa ajili ya timu ya wanaume na leo tunatoa kwa ajili ya wanawake ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya kusapoti soka nchini,” amesema Lydia.

Mtendaji Mkuu wa klabu, Barbara Gonzalez amewawashukuru Africarriers kwa kuendelea kufuata taratibu za makubaliano na kuonyesha thamani ya soka la wanawake.

“Ikiwa tunaendelea kutafuta mdhamini mkuu wa timu yetu ya Simba Queens wenzetu wa Africarriers wameonyesha nia na huenda huko mbele tukakaa mezani tena kuona tunafanyaje.

“Soka la wanawake linazidi kukua, juzi tu tumetoka kuchukua ubingwa wa CECAFA na mwezi wa Oktoba tutaenda kushiriki Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hivyo tunaendelea kuhamasisha makampuni kuja kuwekaza kwetu,” amesema Barbara.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER