Baada ya kucheza mechi mbili mikoani kwa mara ya kwanza leo kikosi chetu kinarejea kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Polisi Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC utakaopigwa saa moja usiku.
Kikosi kinarejea kwa nguvu kwa lengo la kuhakikisha tunacheza soka safi la kuvutia ili kuwaburudisha mashabiki wetu kutokana na matokeo mabaya tuliyopata hivi karibuni.
Baada ya mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwnaneng Galaxy Jumapili kikosi kiliingia kambini moja kwa moja kujiandaa na mechi ya leo dhidi ya Polisi.
Kaimu Kocha Mkuu Hitimana Thierry, amesema licha ya kupata maandalizi ya siku mbili kuelekea mchezo wa leo lakini wachezaji wako tayari kuhakikisha tunarejesha furaha kwa mashabiki.
“Tunachofanya ni kusahau yaliyopita na kuganga yajayo, tumepata siku mbili za kujiandaa na wachezaji wapo tayari kupambana kuhakikisha tunapata pointi tatu muhimu,” amesema Hitimana.
Kwa upande wake mlinzi Erasto Nyoni amewaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi uwanjani ili kutupa sapoti kwa kuwa tunajua wanahitaji furaha.
“Sisi tupo tayari kwa ajili ya mchezo wa leo, ni muhimu kwetu kupata alama tatu lakini tunawaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi kutupa sapoti,” amesema Erasto.
TAARIFA YA KIKOSI
Katika mchezo wa leo tutakosa huduma ya kiungo mkabaji, Taddeo Lwanga ambaye alipata maumivu katika mechi iliyopita na mshambuliaji, Chris Mugalu ambaye anaendelea kuuguza jeraha lake.