Balozi wa Uingereza nchini, David Concar ametembelea ofisi zetu zilizopo Masaki Dar es Salaam kwa lengo la kufahamu mambo mbalimbali ya uendeshaji wa klabu.
Concar amesema yeye ni mfuatiliaji mzuri wa mpira na hilo ni moja ya jambo lililomfanya kutembelea ofisi zetu.
Concar amesema Simba ni moja ya klabu ambazo zinamvutia nchini na anaiona ikizidi kufanya vizuri katika michuano ya ndani na nje.
“Nimefurahi kutembelea klabu ya Simba, mimi ni mfuatiliaji mzuri wa soka ndio maana nimekuja hapa kubadilishana uzoefu na viongozi wa Simba,” amesema Balozi Concar.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema ujio wa Concar umechangiwa na kilichotokea katika ufunguzi wa michuano ya African Football League wiki mbili zilizopita kwakuwa lilikuwa tukio kubwa na kihistoria.
“Kilichotokea katika michuano ya African Football League kimezidi kulitangaza soka la Tanzania, najua haitaishia hapa Balozi Concar itaendelea kwa wenzetu wengine na hii ni faida kwa nchi,” amesema Try Again.
Baada ya kuonana na Viongozi na kuongea na Waandishi wa Habari, Balozi Concar alihudhuria mazoezi ya timu katika Uwanja wa Mo Simba Arena kabla ya kusalimiana na wachezaji.