Leo saa 11 jioni kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC.
Mchezo dhidi ya Yanga haujawahi kuwa mwepesi, mara zote unakuwa na presha kutokana na ukubwa wake.
Maandalizi ya mchezo yamekamilika na kikosi kimepata wiki moja ya mazoezi na wachezaji wapo kwenye hali nzuri.
Robertinho hana presha na Derby…..
Kocha Mkuu Roberto Oliviera ‘Robertinho’ ameweka wazi kuwa hana presha na Derby licha ya kusema inaiheshimu Yanga.
Robertinho amesema anawaamini wachezaji wake kutokana na ubora na uzoefu walionao ambao utatuwezesha kupata pointi tatu.
“Ninawaamini wachezaji wangu, wana vipaji vikubwa na tumejipanga kushinda. Sina presha ya mechi ya leo, ni kama michezo mingine lakini kupata pointi tatu ndicho kipaumbele chetu,” amesema Robertinho.
Kapombe aongea kwa niaba ya wachezaji…..
Mlinzi wa kulia, Shomari Kapombe amesema kila mchezaji anafahamu umuhimu wa ushindi katika mchezo wa leo na yupo tayari kuipigania timu kupata matokeo chanya.
Kapombe amesema wamepata maandalizi mazuri na watafuta maelekezo wakayopewa na benchi la ufundi.
“Kwa upande wetu wachezaji tupo tayari, tumepata wiki moja ya maandalizi ambayo inatufanya tuwe tayari kwa mchezo. Yanga ni timu bora na tunapokutana mechi inakuwa ngumu lakini tumejipanga kuwakabili,” amesema Kapombe.
Tuliwafunga mchezo wa mwisho kwa Mkapa………
Katika mchezo wa mzunguko wa pili wa ligi msimu uliopita uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Aprili 16 tuliibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Katika mchezo huo mabao yetu yalifungwa na mlinzi wa kati, Henock Inonga na Kiungo mshambuliaji, Kibu Denis.
Tuliwafunga Ngao ya Jamii Tanga………
Msimu tayari tumekutana katika mchezo wa Ngao ya Jamii uliofanyika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Agosti 13 na tulishinda kwa penati 3-1 baada ya kutoka suluhu kwenye muda wa kawaida.