Preview: Mchezo wetu dhidi ya Wydad

Leo saa 10 jioni kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Wydad Casablanca katika mchezo wa Robo Fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Tunaingia katika mchezo wa leo tukiwa tunafahamu ugumu na ubora wa wapinzani wetu na tunawaheshimu lakini maandalizi tuliyofanya yanatupa matumaini ya kupata ushindi nyumbani.

Pia tutaingia kwenye mchezo wa leo tukiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi mnono wa mabao 7-0 tuliopata katika mchezo wa mwisho wa Ligi ya Mabingwa tuliocheza nyumbani dhidi ya Horoya kutoka Guinea uliopigwa Machi 18.

Wachezaji wote wako kwenye hali nzuri na wamepata maandalizi ya wiki nzima wakiwa wameandaliwa kimwili na kiakili kuhakikisha ushindi unapatikana leo.

Kocha Mkuu Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema tutaingia kwenye mchezo wa leo kwa lengo moja la kucheza soka safi na kupata ushindi.

“Kwangu mpira wa miguu ni sanaa, tunatakiwa kucheza soka safi na kupata ushindi.

“Lakini pia tumewasisitiza wachezaji wetu kuhakikisha wanacheza vizuri wakiwa wana mpira na wakiupoteza pia. Wydad ni timu bora kama ilivyo Simba, tunaiheshimu lakini tumejipanga kikamilifu kuwakabili,” amesema Robertinho.

Mlinzi wa kulia Shomari Kapombe amesema tumejifunza baada ya kufungwa nyumbani na Raja Casablanca hali ambayo imefanyiwa kazi mazoezini ili isitokee kwa namna yoyote leo.

“Tulipoteza nyumbani dhidi ya Raja lakini tumekuja na mbinu mpya ambazo tunaamini zitatusaidia, tunataka kutumia uwanja wa nyumbani kumaliza mechi kwa kuwa tunajua kule Morocco itakuwa ngumu kwetu,” amesema Kapombe.

Hali ya Kikosi

Manula nje, Kanoute ndani

Mlinda mlango namba moja, Aishi Manula hajafanya mazoezi ya mwisho jana kujiandaa na mchezo wa leo hivyo ndiye mchezaji pekee ambaye tutamkosa katika mchezo wa leo.

Kwa upande wa kiungo mkabaji, Sadio Kanoute ambaye tulimkosa katika mechi kadhaa zilizopita yeye amefanya mazoezi na yupo tayari kwa mchezo wa leo.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER