Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu, Ahmed Ally amesema Jumapili Aprili 17 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kutakuwa na matukio mawili makubwa yakiwemo mashindano ya kimataifa ya kusoma Quran na mchezo wetu wa Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Orlando Pirates.
Kulikuwa na mkanganyiko kuwa itakuwaje baada ya matukio hayo kuingiliana lakini usomaji wa Quran utaanza saa moja asubuhi hadi saa saba ambapo watu watatoka uwanjani ili mashabiki waanze kuingia kushuhudia mechi.
Ahmed amesema kwa kuwa kutakuwa na matumizi ya Video za Usaidizi wa Mwamuzi (VAR) hivyo tutashirikiana na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na warusha matangazo Azam TV kuweka mashine hizo ili kusiwe na changamoto siku ya mchezo.
“Jumapili kutakuwa na mashindano ya kimataifa ya kusoma Quran hadi saa saba mchana na baadaye uwanja utakuwa mtupu na mashabiki wataanza kuingia hivyo mashabiki msiwe na wasiwasi kila kitu kitafanyika siku hiyo.
“Kikubwa mashabiki mjitokeze kwa wingi, sisi kama uongozi tumepambana kuhakikisha tunaruhusiwa na CAF kuujaza uwanja kwa hiyo jitihada hizi msituvunje moyo njooni tuujaze tuwachanganye Orlando,” amesema Ahmed.
Kuelekea mchezo huo Ahmed amesema kesho tutazindua kampeni ya hamasa kwa mashabiki ambayo wenyeji wetu watakuwa Tawi la Tunawakera la Temeke Maduka Mawili, na Jumatano tutakwenda kuhamasisha kwenye Pantoni na Alhamisi tutatembelea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Katika tukio la kesho Mwenyekiti wa klabu, Murtaza Mangungu atakuwa Mgeni rasmi akiongozana na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Mwina Kaduguda ‘Simba wa Yuda’ na mwenyekiti wa zamani, Hassan Dalali .