Kikosi chetu cha timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 kimeibuka na ushindi wa bao moja dhidi ya Mwadui FC katika mchezo wa pili wa hatua ya nane bora.
Mchezo huo uliopigwa katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es Salaam, ulikuwa wa kasi huku timu zikishambuliana kwa zamu ingawa changamoto ilikuwa ni kumalizia nafasi zilizopatikana.
Goli pekee kwenye mchezo huo lilifungwa dakika ya 33 na Samson Lucas baada ya kupokea mpira wa krosi uliopigwa na Baraka Shaban na kuunganisha moja kwa moja mpira uliomshinda mlinda mlango wa Mwadui, Kelvin Kayego.
Baada ya bao hilo timu ziliendelea kulishambuliana kwa zamu huku tukipoteza nafasi kadhaa ambazo zingetufanya kuibuka na ushindi mnono zaidi.
Kocha Nico Kiondo aliwatoa Geodfrey George, Samson Lucas na Omarion Peter na kuwaingiza
Kass Omary, Omarion Peter na Omary Kazi.
Ushindi huu unatufanya kufikisha alama nne tukiwa nafasi ya pili huku tukibakisha mchezo mmoja dhidi ya JKT Tanzania utakaopigwa Jumatatu huku tukitakiwa kushinda ili kujihakikishia kufuzu nusu fainali.
Baada ya mchezo huo Kocha Nico Kiondo amesema wachezaji wetu wamecheza vizuri na dhamira ni kuhakikisha tunashinda kila mchezo ili tuibuke mabingwa wa michuano hii.