Kikosi chetu leo saa 12 jioni kitashuka katika Uwanja wa Majaliwa Ruangwa Mkoani Lindi kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Namungo FC.
Tutaingia kwenye mchezo wa leo tukiwa na kumbukumbu nzuri ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Muungano siku tatu zilizopita Visiwani Zanzibar.
Kikosi kipo kwenye hali nzuri kuelekea mchezo wa leo na lengo letu ni kuhakikisha tunapambana kupata ushindi.
Matola atoa neno kuelekea mchezo wa leo……
Kocha Msaidizi, Selemani Matola amesema mchezo utakuwa mgumu kutokana na ubora wa wapinzani pia Ligi inaelekea ukingoni kwahiyo kila timu inajipanga kuhakikisha inakusanya pointi nyingi hasa kwenye Uwanja wa nyumbani.
Matola amesema tumejiandaa vizuri kuelekea mchezo huo tunafahamu tunaenda kukutana na timu imara lakini tupo tayari kuwakabili na kuchukua pointi zote tatu.
“Utakuwa mchezo mgumu, Namungo ina timu imara yenye wachezaji wazoefu, kwahiyo tunategemea kupata upinzani mkubwa lakini tumejidhatiti kwa ajili ya kupata ushindi,” amesema Matola.
Israel azungumza kwa niaba ya wachezaji.
Akiongeza kwa niaba ya wachezaji mlinzi wa kulia Israel Patrick amesema “tupo tayari kupambana kuhakikisha tunaisaidia timu kupata matokeo mazuri na kuwapa furaha Wanasimba.”
“Haitakuwa mechi rahisi hata kidogo, Namungo ni timu nzuri lakini tumejiandaa kuwakabili na kufuata maelekezo tutakayopewa na walimu,” amesema Israel.
Mechi ya kwanza ya Mgunda….
Kaimu Kocha Mkuu, Juma Mgunda ataiongoza timu kwa mara ya kwanza baada ya kuchukua nafasi ya Abdelhak Benchikha ambaye ameomba kuondoka kutokana na matatizo ya kifamilia.
Nyota watano kuikosa Namungo Leo….
Kocha Msaidizi Seleman Matola ameweka wazi mbele ya Waandishi wa Habari kuwa tutawakosa wachezaji watano kutokana nakuwa majeruhi.
Nyota hao ni Shomari Kapombe, Henock Inonga, Clatous Chama, Luis Miqussone na Ladaki Chasambi.
Kwa upande wa kiungo mkabaji Sadio Kanoute yeye ni 50/50 ingawa ameahiriki mazoezi pamoja na wenzake lakini benchi la ufundi litajiridhisha zaidi kuhusu hali yake na kujua kama yupo tayari kwa ajili ya mchezo wa leo.
Tulitoka sare mara ya mwisho….
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Uhuru, Novemba 9, mwaka jana tulitoka sare ya kufungana bao moja.