Leo saa moja usiku kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Azam FC katika muendelezo wa Ligi Kuu ya NBC.
Mchezo huo mkubwa wenye kuvuta hisia za mashabiki wengi maarufu kama Dabi ya Mzizima haujawahi kuwa mwepesi na hii inatokana na uimara wa timu zote.
Tutaingia kwenye mchezo wa leo tukiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 3-0 tuliopata dhidi ya Namungo FC katika mchezo wa Ligi Kuu uliopigwa Uwanja wa Majaliwa, Jumatano iliyopita.
Fadlu ukiri ugumu wa Dabi
Kocha Mkuu Fadlu Davids amesema mchezo utakuwa mgumu lakini ameweka wazi kuwa kikosi chetu kipo kwenye hali nzuri kupambana na kupata matokeo chanya.
Fadlu ameongeza kuwa kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza tulipata ushindi wa mabao mawili lakini tunaamini Azam watakuja kwa nia ya kutaka kulipa kisasi ndio maana tumewaandaa wachezaji kimbinu na kiakili.
“Maandalizi ya mchezo mkubwa wa Dabi yamekamilika, tumejiandaa vizuri kimbinu za kuikabili timu bora yenye kocha bora ya Azam FC,” amesema Kocha Fadlu.
Zimbwe Jr nae atia neno
Nae nahodha wa timu, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ amesema wachezaji wapo tayari kupambana hadi mwisho kuhakikisha ushindi unapatikana na kuendelea kusogelea malengo tuliyojiwekea.
“Kwa niaba ya wachezaji naweza kusema tupo tayari kwa ajili ya mchezo, haitakuwa mechi rahisi Azam ni timu bora na inapigania ubingwa kama sisi lakini tupo tayari kupambana na kushinda,” amesema Zimbwe Jr.
Kagoma, Mpanzu kucheza Dabi ya kwanza ya Mzizima
Nyota wetu wawili Yusuph Kagoma na Elie Mpanzu leo watacheza mechi ya kwanza ya Dabi ya Mzizima kwakuwa mchezo wa mzunguko wa kwanza hawakuwepo.
Kagoma alikuwa anasumbuliwa na majeraha wakati Mpanzu alikuwa bado hajasajiliwa hivyo leo wataonja joto la Dabi ya Mzizima.
Tuliwafunga Mzunguko wa Kwanza
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Uwanja wa New Amaan Complex Visiwani Zanzibar, Septemba 26 tuliibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Katika mchezo huo mabao yetu yalifungwa na Leonel Ateba na Fabrice Ngoma.