Tupo tayari kwa ‘Dabi’ ya Kariakoo

Leo saa 11 jioni kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC.

Ni mchezo muhimu kwetu kupata alama tatu kwakuwa malengo ni kuhakikisha tunafanya hivyo katika kila mchezo.

Utakuwa mchezo mgumu tunawaheshimu watani kutokana na ubora na aina ya wachezaji walionao lakini tumejipanga kuhakikisha tunapambana kupata pointi zote tatu.

Kauli ya Kocha Fadlu.

Kocha Mkuu, Fadlu Davids amesema maandalizi ya mchezo yamekamilika na wachezaji wapo kwenye hali nzuri kwa ajili ya kuwakabili Yanga.

Kocha Fadlu ameongeza kuwa amekiandaa vizuri kikosi kuelekea mchezo huu wenye presha kubwa huku akiweka wazi kuwa bado matokeo ya mechi hayataamua mbio za ubingwa sababu ligi bado mbichi.

Kuhusu hali ya wachezaji Fadlu amesema “nyota wote waliokuwa kwenye majukumu ya timu za taifa wamerejea kikosini na jana watafanya mazoezi ya mwisho tayari kwa mchezo wa leo. Haitakuwa mechi rahisi lakini tumejipanga kwa ajili ya kupata pointi tatu.”

Wachezaji wanaitaka ‘Dabi’…….

Akiongea kwa niaba ya wachezaji kiungo mshambuliaji, Awesu Awesu amesema wapo tayari kwa ajili ya kupambana hadi mwisho kuhakikisha ushindi unapatikana.

Awesu ameongeza kuwa mchezaji ili uwe bora unatakiwa kufanya vizuri kwenye mechi kubwa kama ya Leo hivyo kila mmoja yupo tayari kuonyesha uwezo wake akipata nafasi.

“Tupo tayari, itakuwa mechi ngumu. Hii ni ‘Dabi’ na siku zote inakuwa na presha kubwa lakini tumapata maandalizi ya kimwili na kiakili kwa ajili ya kufanya vizuri,” amesema Awesu.

Mashabiki waitwa kwa Mkapa

Kwa takribani wiki nzima Meneja Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally amekuwa akiwasisitiza mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanjani kuja kuisapoti timu huku akiwa na imani kubwa ya kupata alama zote tatu.

“Mwanasimba yoyote we njoo kwa Mkapa ukiwa umevaa jezi yako ya Mnyama ninaamini utarejea nyumbani ukiwa na furaha kubwa,” amesema Ahmed.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER