Leo saa 10 jioni kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Kaitaba kuikabili Kagera Sugar katika muendelezo wa Ligi Kuu ya NBC.
Tutaingia katika mchezo wa leo tukiwa tunafahamu kuwa uwanja wa Kaitaba haujawahi kuwa rahisi kwetu na kwa muda mrefu hatujawahi kupata ushindi.
Pamoja na umuhimu wa pointi tatu kwa ajili ya kutaka kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi lakini tunazihitaji kwa ajili ya kuvunja mwiko katika Uwanja wa Kaitaba.
Mara ya mwisho kupata ushindi katika Uwanja wa Kaitaba ilikuwa Aprili 21, 2021 ambapo tulishinda mabao 2-0 ambayo yalifungwa na Chris Mugalu na Luis Miqiussone.
Kocha auzungumzia mchezo kiufundi…..
Kocha Mkuu, Fadlu Davids amesema utakuwa mchezo mgumu huku akiweka wazi kuwa tumekuwa tukipata wakati mgumu katika Uwanja wa Kaitaba lakini leo itakuwa ni vita ya wachezaji 22 na atakayekuwa bora ataondoka na pointi tatu.
Kocha Fadlu amesema historia ipo kwenye mpira lakini tumejipanga kuhakikisha tunaendelea kushinda licha ya ligi kuwa ngumu.
“Tupo tayari kwa mchezo, tunajua Kagera ni timu nzuri na inacheza soka la kisasa na mashambulizi yao yanajengwa kuanzia nyuma lakini tupo tayari kuwakabili,” amesema Kocha Fadlu.
Wachezaji wapo tayari kwa mchezo…..
Kwa upande wake mlinda mlango, Ally Salim amesema pamoja na ukweli kwamba Uwanja wa Kaitaba umekuwa mgumu kwetu kupata pointi tatu lakini wachezaji hawana presha juu ya hilo.
“Tumewahi kukutana na Viwanja vigumu kama ilivyo Kaitaba na bado tuliweza kupata ushindi hata leo tunaweza kufanya hivyo, kikubwa tunahitaji mashabiki wajitojeze kwa wingi kuja kutupa sapoti,” amesema Ally.
Ushindi kuturejesha kileleni…
Pointi tatu kwenye mchezo wa leo utatufanya kufikisha pointi 34 na kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC tukiwa tumecheza mechi 13.