Kikosi chetu leo saa 10 jioni kitashuka katika Uwanja wa KMC Complex kuikabili Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC.
Mchezo dhidi ya Prisons haujawahi kuwa rahisi na mara zote wamekuwa wakitupa upinzani mkubwa hasa unachangiwa na aina ya soka la nguvu wanalocheza.
Tunafahamu umuhimu wa alama tatu katika mchezo wa leo ambao utatufanya kurejea kileleni mwa msimamo hivyo tupo tayari kuzipambania hadi mwisho.
Fadlu akiri ugumu kutoka kwa Prisons
Kocha Mkuu Fadlu Davids ameweka wazi kuwa anaamini utakuwa mchezo mgumu kutokana na Prisons kuwa na kikosi imara huku wakichagizwa na ujio wa kocha mpya.
Fadlu amesema pamoja na ugumu uliopo lakini tutacheza soka letu tulilolizoea na kuhakikisha tunapata mabao ya mapema ili kucheza bila presha.
“Tunategemea utakuwa mgumu, Prisons wana kocha mpya na pia hawako kwenye nafasi nzuri hivyo tumejiandaa kupata upinzani mkubwa lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda,” amesema Fadlu.
Wachezaji wanaitaka mechi….
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji mlinzi wa kulia, Shomari Kapombe amesema pamoja na sare tuliyopata kwenye mchezo uliopita dhidi ya Fountain Gate FC lakini bado malengo yetu ni kupigania ubingwa.
“Sisi kama wachezaji bado hatujakata tamaa na malengo yetu kama tulivyoanza msimu licha ya sare iliyopita lakini tupo tayari kupambana ili kupata alama tatu muhimu,” amesema Kapombe.
Kibu kuikosa Prisons
Kocha Fadlu Davids amesema kiungo mshambuliaji Kibu Denis anaendelea vizuri baada ya kufanyiwa matibabu na ameanza mazoezi mepesi chini ya uangalizi wa daktari hivyo hatakuwa sehemu ya kikosi cha leo.
Tuliwafunga Mzunguko wa Kwanza
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi uliofanyika Uwanja Sokoine jijini Mbeya, Oktoba 22 mwaka jana tuliibuka na ushindi wa bao moja.
Katika mchezo huo uliokuwa mkali bao hilo pekee lilifungwa na mlinzi wa kati Che Fondoh Malone.