Tupo tayari kuikabili Pamba Leo

Leo saa 10 jioni kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa KMC Complex kuikabili Pamba Jiji katika muendelezo wa Ligi Kuu ya NBC.

Tutaingia kwenye mchezo wa leo tukiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa bao moja tuliopata kwenye mechi iliyopita dhidi ya JKT Tanzania.

Ni moja ya mechi ngumu ambazo tunategemea kukutana nayo kutokana na ligi kuelekea ukingoni huku pia wapinzani Pamba wakiwa hawapo kwenye nafasi nzuri.

Hicho ndicho walichosema benchi la ufundi……

Kocha Msaidizi, Seleman Matola amesema maandalizi ya mchezo huo yamekamilika na kikosi chetu kipo kwenye hali nzuri na hakuna mchezaji aliyepata majeraha ambayo yatamfanya kuikosa mechi.

Matola amesema Pamba haiko sehemu salama kwenye msimamo hivyo wanatumia nguvu kubwa katika kila mchezo lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda.

Matola ameongeza kuwa pamoja na ugumu wa mchezo huo lakini tumejipanga vilivyo kuhakikisha tunapata matokeo chanya.

“Utakuwa mchezo mgumu kutokana nafasi waliyopo Pamba lakini Simba ni timu kubwa na inaweza kucheza kwenye mazingira yoyote kwa ajili ya kutafuta pointi tatu,” amesema Matola.

Wachezaji watoa tamko……

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji mlinda mlango, Ally Salim amesema wapo tayari kupambana hadi mwisho kuona alama tatu muhimu zinapatikana.

“Tunafahamu utakuwa mchezo mgumu, Pamba ni timu bora na haipo kwenye nafasi nzuri lakini tumejipanga kupata pointi zote tatu,” amesema Ally.

Tuliwafunga Mzunguko wa Kwanza….

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Uwanja wa CCM Kirumba, Novemba 22 tulishinda kwa bao moja lililofungwa na Leonel Ateba kwa mkwaju wa penati.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER