Tupo tayari kuikabili JKT Tanzania Leo

Leo saa 10 jioni kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo kuikabili JKT Tanzania katika muendelezo wa Ligi Kuu ya NBC.

Tutaingia kwenye mchezo wa leo tukiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 2-1 tuliopata Ijumaa dhidi ya Mashujaa.

Tunategemea kukutana na upinzani mkubwa kutoka kwa JKT Tanzania kutokana na ubora na uzoefu wa kikosi chao lakini tupo tayari kuhakikisha tunapata alama tatu muhimu ugenini.

Hii ndio kauli ya Benchi la Ufundi…..

Kocha Msaidizi, Seleman Matola amesema wachezaji wetu wameandaliwa kimwili na kiakili kucheza mechi hizi za mwisho wakati ligi ikiwa inaelekea ukingoni.

Matola amesema ligi inapokuwa inaelekea mwisho ugumu unaongezeka kwakuwa kila timu inataka kushinda ili kujiweka kwenye nafasi nzuri lakini tupo tayari kupambana na kila kilichopo mbele yetu ili kufikia malengo.

“Haitakuwa mechi rahisi, tunakutana na timu yenye wachezaji wengi wazoefu na wanaijua vizuri ligi lakini Simba ni timu kubwa na tupo tayari kupambana na kila changamoto iliyo mbele yetu,” amesema Matola.

Duchu afunguka kwa niaba ya wachezaji…..

Mlinzi wa kulia David Kameta ‘Duchu’ amesema pamoja na ugumu ambao tunaenda kukutana nao lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda.

“Kila mchezo kwetu ni fainali, Simba ina wachezaji wazuri na wenye uzoefu mkubwa na mechi kama hizi. Tunajua itakuwa mechi ngumu lakini tumejiandaa kuhakikisha tunashinda na kuchukua pointi zote tatu ugenini,” amesema Duchu.

Tuliwafunga Mzunguko wa Kwanza…….

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza tulipokuwa na JKT katika mchezo uliopigwa Disemba 24, 2024 katika Uwanja wa KMC Complex tulipata ushindi wa bao moja.

Bao hilo lilifungwa na kiungo mshambuliaji, Jean Charles Ahoua kwa mkwaju wa penati kufuatia Shomari Kapombe kufanyiwa madhambi ndani ya 18.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER