Tupo tayari kuikabili Fountain Gate FC Leo

Leo saa 10:15 jioni kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa mkoani Manyara kuikabili Fountain Gate FC katika muendelezo wa Ligi Kuu ya NBC.

Tutaingia kwenye mchezo wa leo tukiwa na kumbukumbu nzuri kutokana na ushindi mnono wa mabao 3-0 tuliopata wikiendi iliyopita dhidi ya Tabora United katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.

Tunafahamu utakuwa mchezo mgumu lakini kama ilivyo kawaida tutaingia uwanjani kwa lengo la kutafuta alama tatu muhimu ugenini.

Kauli ya Benchi la Ufundi

Kocha Msaidizi, Darian Wilken amesema mchezo utakuwa mgumu hasa kutokana na Fountain Gate kuwa nyumbani lakini tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunapata alama tatu muhimu ugenini.

Wilken ameongeza kuwa mzunguko wa pili wa ligi ni mgumu na kila timu imejipanga kuhakikisha inafanya vizuri hasa ikiwa nyumbani lakini tumejiandaa kupambana na changamoto yoyote itakayojitokeza.

“Maandalizi yamekamilika, kikosi kimefika leo Manyara na jioni kitafanya mazoezi ya mwisho kwa ajili ya mchezo wa kesho ambao tunaamini utakuwa mgumu,” amesema Wilken.

Nahodha Zimbwe Jr atoa neno

Nahodha wa timu Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ amesema kwa upande wao wachezaji wapo tayari kupambana hadi mwisho kuhakikisha alama tatu zinapatikana.

“Malengo yetu kwenye kila mchezo ni kuhakikisha tunapata alama tatu, kwetu kila mechi ni fainali na tupo tayari kupambana hadi mwisho ili kufanikisha hilo,” amesema Zimbwe Jr.

Tuliwafunga Mzunguko wa Kwanza

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi uliopigwa Agosti, 25, 2024 katika Uwanja wa KMC Complex tuliibuka na ushindi wa mabao 4-0.

Mabao hayo yalifungwa na Edwin Balua, Steven Mukwala, Jean Charles Ahoua na Valentino Mashaka.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER