Leo saa 10 jioni tutashuka katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha kuikabili Coastal Union katika mchezo wa 21 wa Ligi Kuu ya NBC.
Hupatikana moja ya mechi bora kila tunapokutana na Coastal kutokana na aina ya soka tunalocheza.
Malengo yetu kwa sasa ni kuhakikisha tunashinda mechi zetu zote 10 zilizosalia kabla ya kumalizika kwa msimu wa Ligi 2024/25.
Benchi la Ufundi lazungumzia mchezo wenyewe
Akiongea kwa niaba ya benchi la ufundi kocha msaidizi, Seleman Matola amesema tunategemea kupata upinzani mkubwa kutoka Coastal hasa ukizingatia ligi inaelekea ukingoni na kila timu inahitaji kufanya vizuri.
Matola ameongeza kuwa mzunguko wa pili wa ligi kila timu inapambana ili kumaliza kwenye nafasi bora zaidi lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda na kupata alama zote tatu.
“Tumejiandaa vizuri na mchezo dhidi ya Coastal, tumewaandaa wachezaji kimwili na kiakili kuelekea mchezo huo ambao tunafahamu utakuwa mgumu.”
“Mchezo dhidi ya Coastal haujawahi kuwa mwepesi lakini tutahakikisha tunafikia malengo tuliyojiwekea ya kupata pointi tatu kwenye kila mechi iliyobaki,” amesema Matola.
Wachezaji wapo tayari kwa vita ya dakika 90
Kwa niaba ya wachezaji nahodha wa timu, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ amesema tumekuja Arusha kwa lengo moja la kutafuta alama tatu.
“Tumekuja kwenye mchezo huu wa ugenini kutafuta alama tatu hilo ndio jambo muhimu bila kuangalia matokeo yoyote ya nyuma kwani hayo yameshapita,” amesema Zimbwe Jr.
Camara, Che Malone kuikosa Coastal
Mlinda mlango Moussa Camara na mlinzi wa kati Che Fondoh Malone hawatakuwa sehemu ya mchezo wa leo kutokana nakuwa majeruhi.
Tulitoka sare katika mchezo wa mzunguko wa kwanza
Tulipokutana kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Uwanja wa KMC Complex Oktoba, 4, 2024 tulipata sare ya kufungana mabao 2-2.
Katika mchezo huo uliokuwa mkali muda wote mabao yetu yalifungwa na nahodha, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ na Leonel Ateba kwa mkwaju wa penati.