Tupo kibaruani tena kuikabili JKT Tanzania

Leo saa 10 jioni kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa KMC Complex kuikabili JKT Tanzania katika muendeleo wa Ligi Kuu ya NBC.

Hapana shaka mchezo wa leo utakuwa mgumu kutokana na JKT kuundwa na nyota wengi wazoefu ambao walicheza kwenye kikosi chetu kwa nyakati tofauti.

Ligi ni ngumu na timu zimejiandaa vilivyo nasi tumejipanga kuhakikisha tunashinda kwenye kila mchezo.

Matola akubali utakuwa mchezo mgumu….

Kocha Msaidizi Seleman Matola amesema leo tunakutana na JKT ikiwa kwenye ubora mkubwa unaotokana na aina ya wachezaji ilionao.

Matola amesema haijawahi kuwa mechi rahisi kila tunapokutana na JKT Tanzania lakini tumejiandaa kimwili na kiakili kuhakikisha tunapata ushindi.

“Wachezaji wetu wote wapo kwenye hali nzuri kuelekea mchezo dhidi ya JKT, haitakuwa mechi nyepesi lakini dhamira yetu ni pointi tatu hasa ukizingatia tupo nyumbani,” amesema Matola.

Zimbwe awaita mashabiki KMC Complex

Nahodha Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ amewaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi katika Uwanja wa KMC kuipa sapoti timu ili hatimaye tuweze kupata pointi tatu muhimu nyumbani.

Zimbwe amesema mchezo utakuwa mgumu lakini maandalizi tuliyopata kutoka kwa benchi la ufundi pamoja na nguvu ya mashabiki tutaweza kupata ushindi.

“Kikubwa tunahitaji mashabiki wetu kujitokeza kwa wingi uwanjani kuja kutupa sapoti tunaamini tutapata ushindi,” amesema Zimbwe Jr.

Mechi ya kwanza Mpanzu  nyumbani

Baada ya kuonyesha kiwango safi katika mchezo wa ugenini dhidi ya Kagera Sugar leo kiungo mshambuliaji, Elie Mpanzu atacheza mechi ya kwanza ya nyumbani.

Usajili wa Mpanzu ulichelewa hivyo ilibidi asubiri hadi kufunguliwa kwa dirisha dogo Disemba 15 ili kuweza kuitumikia Simba na tayari ameanza kuonyesha makali yake kwenye mchezo dhidi ya Kagera siku ya Jumamosi.

Tuliwafunga 2-0 tulipokutana mara ya mwisho

Katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi msimu uliopita ambao ulichezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Mei 28, 2024 tuliibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Mabao yetu yalifungwa na Saido Ntibazonkiza kwa mkwaju wa penati na Leandro Essomba Onana

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER