Tupo Kamili Kuivaa Al Masry Leo

Leo saa moja usiku kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Suez nchini Misri kuikabili Al Masry katika mchezo wa robo fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Ni moja ya mechi ngumu ambayo tunatarajia kucheza usiku wa leo hasa tukifahamu wapinzani wetu Al Masry watataka kuutumia vizuri uwanja wa nyumbani lakini tumejipanga kuhakikisha tunapata matokeo chanya dhidi yao.

Tutaingia katika mchezo wa leo kwa nidhamu kubwa hasa katika ulinzi huku wachezaji wakisisitizwa kutumia vema nafasi zinazopatikana ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu nusu fainali.

Hichi ndicho alichosema Kocha Fadlu….

Benchi letu la ufundi limeweka wazi kuwa wachezaji wameandaliwa kimwili na kiakili kuhakikisha wanacheza bila presha ili kufanikisha malengo tuliyojiwekea.

Kauli hiyo imetolewa na Kocha Mkuu Fadlu Davids ambapo amekiri kuwa utakuwa mchezo mgumu lakini tumejiandaa kuhakikisha tunafanya vizuri.

Fadlu ameongeza kuwa anajua mechi ya pili itakayopigwa jijini Dar es Salaam ndio itaamua nani wa kufuzu nusu fainali lakini mipango yetu ni kuhakikisha tunafanya vizuri leo ili kuweka mazingira rafiki kwa mchezo ujao.

“Itakuwa mechi ngumu, lakini tumejiandaa vizuri. Kikosi chetu kimepata muda mzuri wa maandalizi na tumefanya mazoezi hapa Misri kwa siku nne na tupo tayari kwa mchezo,” amesema Fadlu.

Wachezaji wanaitaka mechi……

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji mshambuliaji, Steven Mukwala amesema wapo tayari kuhakikisha wanapigania nembo ya klabu ili kufanikisha malengo ya kutinga nusu fainali.

“Kwa upande wetu wachezaji tupo tayari kuhakikisha tunapambana kwa dakika zote 90 ili kuwapa furaha Wanasimba wote ambao tunaamini watakuwa nyuma yetu,” amesema Mukwala.

Tumedhamiria kuvuka nusu fainali msimu huu…

Hii ni robo fainali ya sita kwetu kwenye michuano ya Afrika (Klabu Bingwa na Kombe la Shirikisho) katika kipindi cha miaka saba iliyopita lakini hatukuweza kuvuka.

Kutokana na ubora na aina ya wachezaji tulionao tunaamini safari hii tunavuka na kutinga nusu fainali.

Ni mechi ya kisasi….

Machi 7/2018 tukikutana na Al Masry katika mchezo wa hatua ya awali uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa na tukatoka sare ya kufungana mabao 2-2 na tulivyorudiana Machi 17/2018 tukatoka sare ya bila kufungana wakatutoa

Safari tumedhamiria kuhakikisha tunalipa kisasi na kuwatupa Al Masry nje ya mashindano.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER