Leo saa 10 jioni kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa KMC Complex kuikabili KMC FC katika muendelezo wa Ligi Kuu ya NBC.
Tutaingia kwenye mchezo wa leo tukiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 5-1 tuliopata dhidi ya Pamba katika mchezo wa Ligi Kuu uliopigwa siku ya Alhamisi.
Tunafahamu utakuwa mchezo mgumu na tunategemea kupata upinzani mkubwa lakini tumejiandaa na tupo tayari kuhakikisha tunapambana mpaka dakika ya mwisho kupata alama tatu.
Alichosema Kocha Matola kuelekea mchezo wa leo
Kocha Msaidizi, Matola amesema pamoja na ubora walionao KMC lakini bado hawapo nafasi nzuri kwenye msimamo hivyo lazima wapambane kutafuta alama tatu katika uwanja wa nyumbani ingawa tupo tayari kuwakabili.
Matola ameongeza kuwa ratiba yetu ni ngumu kutokana na kucheza mechi kila baada ya siku mbili ndio maana tumekuwa tukifanya mabadiliko ya kikosi mara kwa mara.
“Nikiri tu tuna ratiba ngumu, hatupati muda mwingi wa maandalizi lakini tuna kikosi kipana ambacho kinaweza kutuwezesha kupata ushindi popote. Tunategemea kupata upinzani mkubwa kutoka kwa KMC lakini tumejipanga kupata matokeo chanya,” amesema Matola.
Wachezaji wapo tayari kwa mchezo…..
Akiongea kwa niaba ya wachezaji mlinda mlango, Hussein Abel amesema pamoja na ugumu ambao tunatarajia kukutananao lakini tumejipanga kupambana hadi mwisho kupata pointi tatu.
“Mchezo utakuwa mgumu KMC ni timu imara yenye wachezaji wazuri, tunategemea kupata upinzani mkubwa lakini Simba ni kubwa na tutaingia kwa malengo ya kupata pointi tatu,” amesema Abel.
Tuliwafunga Mzunguko wa Kwanza……
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Uwanja wa KMC Complex, Novemba 6, tuliibuka na ushindi wa mabao 4-0.
Mabao hayo yalifungwa na Awesu Awesu, Jean Charles Ahoua aliyefunga mawili na Edwin Balua.