Leo saa 10 jioni kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Dodoma Jiji.
Tunaingia kwenye mchezo wa leo tukiwa tunafahamu utakuwa mchezo mgumu kutokana na ubora wa Dodoma lakini tupo tayari kupambana.
Pointi tatu kwenye mchezo wa leo ni muhimu kwetu kwakuwa lengo letu kwa sasa tunahitaji kumaliza nafasi ya pili ili kujiweka kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Alichosema Mgunda ni hiki…….
Kaimu Kocha Mkuu, Juma Mgunda amesema maandalizi yamekamilika na kikosi kipo tayari kwa ajili ya mchezo na tunajua tutapata ugumu lakini tupo tayari.
Mgunda amesema kikosi kipo kwenye hali nzuri na kimepata muda wa kufanya mazoezi ya kujiandaa na tunategemea utakuwa mgumu kutokana na ubora wa Dodoma.
“Maandalizi ya mchezo ya kucheza na timu bora yamekamilika, tunaamini utakuwa mgumu lakini tupo tayari,” amesema Mgunda.
Ntibazonkiza, Ngoma warejea…….
Kiungo mshambuliaji Saido Ntibazonkiza ambaye alikuwa majeruhi na kukosa zaidi ya mechi mbili amepona na sasa yupo tayari kwa mchezo wa leo.
Ntibazonkiza yupo pamoja na kikosi jijini Dodoma na amefanya mazoezi ya mwisho jana pamoja na wenzake na yupo tayari kwa mchezo wa leo.
Kiungo mkabaji Fabrice Ngoma ambaye alikosekana katika mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar kutokana na kutumikia adhabu ya kadi tatu za njano nae yupo tayari kwa mtanange wa leo.
Tuliwafunga katika mchezo uliopita……
Katika mchezo wa Mzunguko wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam Agosti 20 tuliibuka na na ushindi wa mabao 2-0.
Katika mchezo huo mabao yetu yalifungwa na Jean Baleke na Moses Phiri.