Tunataka kukamilisha mzunguko wa kwanza Ligi kuu tukiwa kileleni

Leo saa 10 jioni kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Liti mkoani Singida kwa ajili ya kuikabili Singida Black Stars kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC.

Mchezo wa leo ni wa 15 ambao unakamilisha mzunguko wa kwanza wa Ligi.

Mpaka sasa tupo kileleni mwa msimamo tukiwa na alama 37 na endapo tutashinda mechi ya leo tutafikisha 40 ambazo hata timu nyingine zikicheza mechi zao haziwezi kufikia.

Hiki ndicho alichosema kocha Fadlu….

Kocha Mkuu, Fadlu Davids ameweka wazi kuwa mchezo utakuwa mgumu lakini tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunafanya vizuri na kuondoka na alama zote tatu ugenini.

Kocha Fadlu amesema kikosi kipo kwenye hali nzuri na tumepata siku mbili kwa ajili ya mazoezi tangu tulivyocheza mechi ya mwisho dhidi JKT Tanzania.

“Maandalizi ya mchezo yamekamilika, jana jioni tumefanya mazoezi ya mwisho katika Uwanja wa Liti na wachezaji wote wapo timamu kwa mchezo,” amesema Fadlu.

Wachezaji wapo kamili……

Akizungumzia kwa niaba ya wachezaji kiungo mshambuliaji, Awesu Awesu amesema kila mmoja anafahamu umuhimu wa mchezo wa leo na yupo tayari kupambana ili timu kupata ushindi.

“Kwa upande wetu wachezaji tupo tayari kupambana hadi mwisho kuhakikisha tunapata matokeo ya alama tatu ugenini,” amesema Fadlu.

Kagoma: Nitafurahi kuisaidia timu kupata ushindi

Kiungo mkabaji, Yusuph Kagoma ambaye msimu uliopita alikuwa Singida Black Stars amesema itakuwa furaha kwake kama ataisaidia timu kupata alama tatu leo.

“Singida ni timu iliyonipa heshima kubwa lakini sasa nipo Simba hivyo nitahakikisha napambana mpaka mwisho kuisaidia timu kupata ushindi na hiyo itakuwa furaha kubwa kwangu,” amesema Kagoma.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER