Kikosi chetu leo saa 10 jioni kitashuka katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kuikabili Coastal Union kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC.
Tunaingia katika mchezo wa leo tukiwa na kumbukumbu nzuri ya kushinda mechi mbili za ligi za mwanzo dhidi ya Mtibwa Sugar na Dodoma Jiji.
Mchezo wa leo ni wa pili wa nyumbani hivyo kupambania pointi tatu ndio kipaumbele chetu cha kwanza.
Tuna kumbukumbu nzuri kwani mchezo wetu wa mwisho tuliocheza Uwanja wa Uhuru, Septemba 20 tuliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Dodoma Jiji.
Robertinho azitaka pointi tatu za Coastal
Licha ya kukiri utakuwa mchezo mgumu lakini Robertinho amesema lengo letu ni kuhakikisha tunacheza soka safi na kushinda.
Robertinho ameongeza kuwa tunaiheshimu Coastal kutokana na ubora walionao lakini tupo tayari kupambana mpaka mwisho ili tupate alama tatu.
“Tupo tayari kwa mchezo wa leo, Sisi kila mpinzani tunamuheshimu na tunafahamu itakuwa mechi ngumu lakini tunahitaji kupata alama tatu.”
“Haitakuwa mechi rahisi kwakuwa Coastal wana kikosi kizuri, nawaamini wachezaji wangu na siku zote tunaingia uwanjani kwa lengo la kucheza soka safi na kushinda,” amesema Robertinho.
Tuliwafunga 3-1 mara ya mwisho
Katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu uliopigwa Uwanja wa Uhuru msimu uliopita tuliifunga Coastal mabao 3-1.
Mabao yetu yalifungwa na Said Ntibazonkiza aliyefunga mawili na nahodha John Bocco huku lile la Coastal likifungwa na Mubarak Amza kwa mkwaju wa penati.