Tunarejea NBC kwa kuanza na Mashujaa Leo

Baada ya mapumziko ya takribani mwezi mmoja wa kusimama Ligi Kuu ya NBC kupisha michuano ya Mapinduzi na AFCON kikosi chetu leo kinarejea kuikabili Mashujaa FC katika mchezo utakaopigwa katika  Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.

Mara ya mwisho kikosi chetu kucheza mechi ya ligi ilikuwa Disemba 23 tulipotoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya KMC katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Mechi ya leo ni ya 11 msimu huu huku tukiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo baada ya kukusanya pointi 23.

Kauli ya Matola kuhusu mchezo wa leo…..

Kocha Msaidizi Seleman Matola amesema mchezo utakuwa mgumu kutokana na wenjeji Mashujaa kutokuwa katika nafasi nzuri hivyo watapambana kwa kila hali kuhakikisha wanashinda nyumbani lakini hata hivyo tumejipanga kuwakabili.

“Tunajua haitakuwa mechi rahisi, Mashujaa imefanya usajili mzuri na wachezaji wengi ni wazoefu wa ligi lakini tumejipanga kuwakabili na lengo ni kupata pointi tatu,” amesema Matola.

Kuhusu hali ya kikosi Matola amesema “wachezaji wote tuliosafiri nao wapo kwenye hali nzuri hakuna aliyepata majeruhi ambayo yatamfanya kuukosa mchezo.”

Nyota sita kucheza mechi ya kwanza ya Ligi

Wachezaji wetu sita tuliowasajili katika dirisha dogo la usajili watakuwa wanacheza mechi ya kwanza wakiwa na kikosi chetu.

Nyota hao ni Saleh Karabaka, Babacar Sarr, Ladack Chasambi, Pa Omar Jobe, Fred Michael Kouablan na Edwin Balua.

Nyota hawa wamecheza mechi za Kombe la Mapinduzi na mchezo wa hatua ya 64 bora ya Azam Sports Federation Cup tulipoifunga 4-0 Tembo FC lakini kwenye Ligi Kuu ya NBC leo itakuwa ya kwanza.

Chama arejea kikosini

Kiungo mshambuliaji, Clatous Chama amejiunga na kikosi baada ya kusamehewa adhabu ya utovu wa nidhamu.

Chama amekuja jana mchana kutoka jijini Dar es Salaam na jioni amefanya mazoezi ya mwisho na wenzake na kama kocha Abdelhak Benchikha ataona inafaa atampa nafasi katika mchezo wa leo.

Mechi ya kwanza ya Ligi dhidi ya Mashujaa.

Mchezo wa leo ni kwanza wa Ligi Kuu tunakutana na Mashujaa baada ya kupanda Ligi kuu msimu huu.

Mara ya mwisho tulichukua Kombe Lake Tanganyika

Mchezo wetu wa mwisho kucheza katika Uwanja wa Lake Tanganyika ilikuwa Julai 25 mwaka 2021 tuliipocheza na watani Yanga mchezo wa fainali ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) tukaibuka na ushindi wa bao moja lililofungwa na kiungo mkabaji, Taddeo Lwanga.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER