Kikosi chetu leo kitashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Nyasa Big Bullets ya Malawi katika mchezo wa marudiano wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaonza saa 10 jioni.
Tutaingia kwenye mchezo wa leo tukiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 2-0 tuliopata kwenye mechi ya mkondo wa kwanza iliyopigwa katika Uwanja wa Bingu Mutharika nchini Malawi, Jumamosi iliyopita.
Pamoja na ushindi tuliopata kwenye mchezo wa kwanza hatutaingia kwa kuwadharau Big Bullets badala yake tutahakikisha tunafanya kila linalowezekana kushinda.
KAULI YA KOCHA MGUNDA
Kocha Mkuu Juma Mgunda, amesema kikosi kipo tayari, wachezaji wapo kwenye hali nzuri na wamefanya mazoezi ya mwisho jana tayari kwa mchezo wa leo.
Mgunda amesema bado hatujafuzu tunahitaji kupambana na kutobweteka na matokeo ya mchezo wa kwanza hivyo amewasisitiza wachezaji kuhakikisha wanapambana ili kuwapa furaha Wanasimba.
“Maandalizi ya mchezo yamekamilika kikubwa tuwaombee wachezaji watimize majukumu yao tuliyo waelekeza, tunaamini utakuwa mchezo mgumu lakini tupo tayari kuhakikisha tunafanya vizuri na kuingia hatua inayofuata,” amesema Mgunda.
ZIMBWE JR AWASHUKURU MASHABIKI
Nahodha Msaidizi Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ amewashukuru mashabiki wetu kwakuwa karibu na timu wakati wote kitu ambacho kinawapa hamasa kubwa kupambana kutafuta ushindi.
“Mashabiki wetu ni watu muhimu sana, wanakuja kila mechi uwanjani kuna waliosafiri hadi Malawi ili kuja kutupa sapoti, tunathamini sana mchango wenu na lengo letu ni kuwafurahisha kwenye kila mchezo,” amesema Zimbwe Jr.
KANOUTE AREJEA MZIGONI
Kiungo mkabaji Sadio Kanoute amerejea kikosini baada ya kuukosa mchezo wa ligi dhidi ya Tanzania Prisons.