Kikosi chetu leo saa moja usiku kitashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Mtibwa Sugar katika mchezo wa mwisho wa kufungia msimu tukiwa nyumbani.
Baada ya mchezo wa leo tutasafiri kuelekea Nyanda za Juu Kusini kwa ajili ya mechi mbili za kukamilisha msimu dhidi ya Tanzania Prisons na Mbeya Kwanza.
Kama ambavyo tumekuwa tukisema kila siku lengo letu ni kuwapa furaha mashabiki wetu kwa kuhakikisha tunashinda kila mchezo uliopo mbele yetu.
ALICHOSEMA KOCHA MATOLA
Kaimu Kocha Mkuu, Seleman Matola amesema mchezo utakuwa mgumu Mtibwa ni timu bora na haipo kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo lakini tupo tayari kupambana kubakisha alama tatu nyumbani.
Matola amesema kikosi kipo kwenye hali nzuri, morali ya wachezaji ipo juu na tunasisitiza tunahitaji kushinda katika kila mchezo uliopo mbele yetu.
“Mchezo utakuwa mgumu, Mtibwa ni timu nzuri na haipo katika nafasi nzuri kwenye msimamo hivyo watataka kuhakikisha wanapata pointi tatu kutoka kwetu lakini tupo tayari kuwakabili,” amesema Matola.
WAWA KUAGWA RASMI LEO
Mlinzi wa kati wa Kimataifa, Pascal Wawa leo atacheza mechi ya mwisho akiwa na kikosi chetu baada ya kumaliza mkataba wake baada ya kudumu nasi miaka mitano.
Kutokana na mchango na ubora wake aliouonyesha katika kipindi chote cha miaka mitano kikosini uongozi wa klabu umeamua kumuaga kwa heshima mbele ya mashabiki wetu.
BARBARA KUWAAGA MASHABIKI DAR
Mtendaji Mkuu wa Klabu, Barbara Gonzalez atatembelea vikundi vyote vya hamasa uwanjani kutoa Shukrani kwa mashabiki wa jijini Dar es Salaam kutokana na mchango wao na kuwa pamoja na timu kwenye nyakati zote msimu huu.
Mara zote mashabiki ni watu muhimu sana na wana mchango mkubwa kwenye mafanikio ya timu nasi tunaitambua thamani yao ndiyo maana nasi leo tunawaaga rasmi katika mchezo wetu wa mwisho wa nyumbani.