Kikosi chetu leo saa tano usiku kitashuka katika Uwanja wa Cairo International kuikabili Al Ahly katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mchezo wa leo ni kama fainali kwetu kwakuwa tunahitaji kushinda zaidi ya mabao mawili ili kutinga nusu fainali.
Tunakubali tuna kibarua kigumu kutokana ubora wa Al Ahly lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda na kufuzu kwenda hatua ya nusu fainali.
Benchikha: Hatuwahofii Al Ahly……
Kocha Mkuu, Abdelhak Benchikha amesema tutaingia kwenye mchezo wa leo tukiwa hatuna hofu yoyote na tutacheza kwa mipango yetu bila kushinikizwa na wapinzani.
Benchikha ameongeza kuwa tumekuja Misri kushindana na tunajua mechi itakua ngumu lakini amewaambia wachezaji watumie kila nafasi watakayopata kuhakikisha tunafunga mabao.
“Hatujaja kufungwa hapa Misri, kama tungejua tunakuja kufungwa tusingekuja kabisa, tumekuja kushindana wala hatuhofii chochote. Itakuwa mechi ngumu lakini tumejipanga kuwakabili,” amesema Benchikha.
Che Malone atoa neno……..
Mlinzi wa kati, Che Fondoh Malone amesema licha ya kucheza ugenini bila mashabiki wetu lakini tumejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri.
“Kuna tofauti ya kucheza nyumbani na ugenini lakini mpira ni ule ule mashabiki wao hawawezi kutuathiri chochote, sisi tutajikita na yale yanayotokea Uwanjani tuu,”: amesema Che Malone.
Tunataka kulipa kisasi Misri……….
Mchezo wa mkondo wa kwanza tuliocheza Machi 29 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa tulipoteza kwa bao moja sasa tunataka kushinda ili kulipa kisasi.
Mayele atung’ata sikio kuhusu Al Ahly……
Mshambuliaji wa Pyramids, Fiston Mayele amesema tunayo nafasi ya kufuzu nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kama wachezaji watajituma na kutumia vizuri nafasi tutakazopata.
“Kwenye mpira kila kitu kinawezekana, Al Ahly haipo kwenye ubora wake wa zamani kwahiyo Simba inaweza kushinda hapa Misri na naipa nafasi ya kufanya hivyo,” amesema Mayele.