Tuna kibarua kigumu dhidi ya CS Sfaxien usiku wa leo

Kikosi chetu leo saa moja usiku kitashuka katika Uwanja Hammadi Agrebi – Tunis kwa ajili ya kuikabili CS Sfaxien katika mchezo wa nne wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Ni mchezo muhimu na mgumu kwetu kutokana na wenyeji wetu Sfaxien kuhitaji alama tatu ili kufufua matumaini ya kutinga robo fainali.

Pamoja na ugumu ambao tunategemea utakuwepo lakini kikosi chetu kipo tayari kuhakikisha tunapambana ili kupata alama tatu ugenini.

Fadlu akiri ugumu wa mchezo…..

Kocha Mkuu Fadlu Davids amesema mchezo utakuwa mgumu kwanza akisema Sfaxien wana kikosi bora chenye mchanganyiko wa vijana na wazoefu, pili akiweka wazi kuwa ni mechi ya ugenini hivyo anategemea ugumu utakuwepo.

Fadlu ameongeza kuwa kwenye michuano hii kila timu huwa inapambana kuhakikisha inashinda mechi za nyumbani lakini tumejiandaa kimwili na kiakili kuhakikisha tunafanya vizuri.

“Utakuwa mchezo mgumu, ikifika hatua hii kila mchezo unakuwa mgumu hasa ukiwa ugenini lakini tumejiandaa kuhakikisha tunapata matokeo chanya,” amesema Kocha Fadlu.

Wachezaji wanaitaka mechi….

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji mlinzi wa kati, Che Fondoh Malone amesema wachezaji wanafahamu umuhimu wa kupata ushindi kwenye mechi ya leo ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu robo fainali.

“Tunajua tupo ugenini na haitakuwa mechi nyepesi lakini tumejiandaa vizuri na tupo tayari kwa mapambano,” amesema Che Malone.

Mpanzu kucheza mechi ya kwanza leo….

Kiungo mshambuliaji, Elie Mpanzu leo atacheza mechi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuidhinisha usajili wake.

Mechi kupigwa bila mashabiki…..

Faida kubwa ambayo tutakuwa nayo kwenye mchezo wa leo ni kuchezwa bila mashabiki baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuifungia Sfaxien kutokana na vitendo vya vurugu uwanjani.

Pia mchezo wa leo utapigwa katika mji wa Tunis na sio Sfaxien wanapotoka wapinzani hivyo bado itakuwa faida pia kwetu.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER