Baada ya ushindi wa mabao 3-0 tuliopata Alhamisi dhidi ya Mbeya City leo tunashuka tena katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili KMC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC.
Wachezaji wapo kwenye hali nzuri na jambo jema hatukupata majeraha katika mchezo uliopita kwa hiyo Kaimu Kocha Mkuu, Seleman Matola atakuwa na nafasi kubwa ya kufanya uchaguzi wa kikosi.
Matola ameendelea kusisitiza kuwa tunahitaji kushinda katika kila mchezo ulio mbele yetu kwa ajili ya kuweka heshima baada ya kuukosa ubingwa.
“Mchezo utakuwa mgumu na tunaiheshimu KMC lakini tumejipanga kuhakikisha tunabaki na alama zote tatu. Pointi tatu katika kila mchezo uliobaki ndiyo lengo tuliojiwekea, tunataka kumaliza ligi kwa heshima. Hata kama tumekosa ubingwa lakini tunataka kuwapa furaha mashabiki wetu kwenye mechi zilizobaki,” amesema Matola.
CHAMA KUWAKOSA KMC
Kiungo mshambuliaji Clatous Chama, hatakuwa sehemu ya mchezo wa leo kwa kuwa hayupo fiti asilimia 100 ingawa tayari ameanza kufanya mazoezi na wenzake.