Kikosi chetu kimefanikiwa kutinga robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuifunga Horoya FC mabao 7-0 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa huku kiungo mshambuliaji Clatous Chama akipiga hat trick.
Chama alitupatia bao la kwanza dakika ya 10 kwa shuti kali la mpira wa adhabu nje ya 18 baada ya Jean Baleke kufanyiwa madhambi.
Baleke alitupatia bao la pili dakika ya 32 baada ya shuti kali lililopigwa na Kibu Denis kupanguliwa na mlinda mlango wa Horoya kabla ya kumkuta mfungaji.
Chama alitupatia bao la tatu kwa mkwaju wa penati dakika ya 36 baada ya mlinzi wa Horoya Abdoulaye Camara kuunawa mpira ndani ya 18.
Kipindi cha pili tulirudi kwa kasi ambapo dakika ya 53 Kiungo Sadio Kanoute alitupatia bao la nne akipokea pasi ya upendo kutoka kwa Chama.
Baleke aliongeza bao la tano dakika ya 65 kufuatia Chama kumpoka mpira mchezaji wa Horoya kabla ya kumkuta mfungaji ambaye alimchambua mlinda mlango.
Chama alitupatia bao la sita dakika 70 na kukamilisha hat trick yake baada ya kumlamba chenga mlinzi wa Horoya ndani ya 18 akimalizia pasi safi kutoka kwa Pape Sakho.
Kanoute alipigilia msumari wa moto wa saba kwa shuti kali nje ya 18 dakika ya 86 akimalizia pasi ya upendo kutoka Shomari Kapombe.
X1: Manula, Kapombe, Zimbwe Jr, Onyango, Henock (Kennedy 88) Kanoute, Chama, Mzamiru (Erasto 84′), Baleke (Phiri 84′), Ntibazonkiza, Kibu (Sakho 56′)
Walionyeshwa kadi: Kibu 29′ Mzamiru 35′ Sakho 59′
X1: Kamara (Syla 45′), Samake, Diaw, Coullibaly, Fofana, Djibo, Soumah (Yakhouba 45′), Camara (Kante 60), Douda (Soumah 60′), Ndiaye, Camara
Walionyeshwa kadi: Abdoulaye Camara 35′ Coullibaly 77′