Baada ya kumalizika rasmi kwa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ambayo tulicheza fainali sasa tumerejea Ligi Kuu ya NBC na leo saa 10 jioni tutavaana na Singida Black Stars katika Uwanja wa KMC Complex.
Kwa sasa tumeelekeza nguvu zetu kwenye michuano hii na lengo letu ni kuhakikisha tunapambana muda wote ili kupata matokeo chanya.
Tunafahamu utakuwa mchezo mgumu na tunaiheshimu Singida kutokana na ubora walionao lakini tupo tayari kuwakabili na kupata alama tatu.
Hichi ndicho alichosema Kocha Matola…..
Kocha Msaidizi, Seleman Matola ameweka bayana kuwa Singida ni timu imara na tunategemea kupata upinzani mkubwa lakini hata hivyo tumejipanga vizuri kuhakikisha tunachukua alama zote tatu nyumbani.
“Tunafahamu tuenda kucheza mechi ngumu kesho, Singida Black Stars ni timu bora na ina kikosi imara na hizi ni mechi za mwisho za kuamua ubingwa tumejipanga kuhakikisha tunapata matokeo ya ushindi,” amesema Matola.
Duchu atoa neno…..
Mlinzi wa kulia, David Kameta ‘Duchu’ akizungumza kwa niaba ya wachezaji amesema pamoja na ubora walionao Singida lakini tupo tayari kupambana mpaka mwisho ili kupata alama tatu.
“Sisi kama wachezaji tumejiandaa kuhakikisha tunashinda nakuchukua alama tatu, kucheza mechi mbili ndani ya siku nne haitakuwa changamoto ya kushindwa kupata ushindi kesho tupo tayari na tumejipanga,” amesema ‘Duchu’.
Tuliwafunga Liti……
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Liti tuliibuka na ushindi wa bao moja lililofungwa na Fabrice Ngoma.