Tumepoteza alama tatu ugenini

Mchezo wetu wa tano wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya ASEC Mimosas uliopigwa Uwanja wa Generali Mathieu Karekou nchini Benin umemalizika kwa kupoteza kwa mabao 3-0.

Wenyeji ASEC walipata bao la kwanza dakika ya 15 kupitia kwa Kramo Aubin akimalizia mpira wa krosi uliopigwa na Oura Anicet kutoka upande wa kulia.

ASEC waliongeza bao la pili dakika ya 24 kupitia kwa Stephano Aziz Ki kwa shuti kali la mguu wa kushoto lililomshinda mlinda mlango Aishi Manula.

Dakika ya 35 Manula aliokoa mkwaju wa penati uliopigwa na Karim Konate baada ya yeye mwenyewe kumfanyia madhambi Kramo ndani ya 18.

Kipindi cha pili kocha Pablo Franco aliwatoa Mzamiru Yassin, Kibu Denis, Rally Bwalya, Jonas Mkude na Henock Inonga kuwaingiza Peter Banda, Bernard Morrison, Taddeo Lwanga, Chris Mugalu na Pascal Wawa ambao waliongeza kasi na kutufanya kucheza kwa utulivu.

Konate aliwapatia wenyeji bao la tatu dakika ya 56 kwa kichwa akimalizia mpira wa krosi uliopigwa na mlinzi wa kulia Kwasi Attohoula.

Dakika ya 89 Manula aliokoa penati nyingine iliyopigwa na Oura Anicet kufuatia Joash Onyango kumfanyia madhambi Konate ndani ya 18.

Licha ya kupoteza mchezo wa leo bado tuna nafasi ya kuingia robo fainali kama tutapata ushindi kwenye mechi ya mwisho ya nyumbani dhidi ya US Gendarmerie.

SHARE :
Facebook
Twitter

2 Responses

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER