Tumefanya maajabu mengi na Jumapili haitakuwa kitu kipya

Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu, Ahmed Ally amesema katika miaka ya karibuni tumewahi kufanya maajabu makubwa ya kupindua matokeo ambayo wengi walidhani haitawezekana tena tukiwa katika mazingira magumu.

Ahmed amesema hata sio zamani msimu huu kila timu ambayo iliwahi kutufunga nyumbani kwao nasi tuliwafunga kwetu kwahiyo Wanasimba wala msiwe na hofu kikubwa tuendelee na mshikamano na kila mmoja wetu aone ana jukumu lakuhakikisha timu inabeba ubingwa.

“Simba tumeshafanya maajabu mengi acha ya zamani, msimu huu kila aliyetufunga na sisi tulimfunga. Berkane ameshamaliza zamu yake sasa ni zamu yetu. Hatuzungumzi haya sababu ya historia bali ubora ambao tupo nao.”

“Tunakubali Benjamin Mkapa ndio ngome yetu lakini hatushindi sababu ya uwanja, tunashinda sababu ya ubora wetu. Uwanja wa Amaan ndio ulitupeleka fainali na sasa ndio utatupa ubingwa. Hatukulipa deni mbele ya Hayati Rais Ally Hassan Mwinyi na sasa tunakwenda kulipa deni mbele ya mtoto wake, Rais Dkt. Hussein Mwinyi,” amesema Ahmed.

Akizungumza kuhusu figisu za nje ya uwanja ili tushindwe kuchukua ubingwa Ahmed amesema vita ni kubwa lakini tunaendelea kupigana na taji hili tunabeba.

“Tunafahamu kuna watu wanafanya kila hila mnyama asichukue ubingwa lakini ifanye kwa kificho, tukikuona hatutakuacha salama. Hapa tulipo tumevua kabisa vazi la utu, tumevua vazi la ustaarabu, hapa tumelipo tumevaa unyama kwelikweli, tusitafutiane lawama. Hatutamuonea mtu aibu, tutakuharibia mazima.”

“Sisi tumeshatabiriwa na Hayati Rais Dkt. John Magufuli kwamba sisi ndio tutakuwa wa kwanza kuleta ubingwa wa Afrika twendeni tukakamilishe ndoto hiyo,” amesema Ahmed.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER