Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ amefunguka kuwa tutatengeneza kikosi imara na benchi bora la ufundi kuelekea Msimu Mpya wa Ligi 2022/23.
Try Again amesema ameongea na Rais wa Heshima wa Klabu Mohamed Dewji ‘Mo’ ambaye amemuahidi atatoa kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya usajili wa wachezaji ambao watakuwa na umri sahihi pamoja na uwezo mkubwa.
Mwenyekiti huyo amesema kikosi kilichopo kitafanyiwa mabadiliko makubwa ambapo kuna wachezaji ambao wataruhusiwa kuondoka huku wengine wakipelekwa kwa mkopo kwenye timu nyingine lakini kwa maridhiano ili kutoa nafasi ya kusajili wapya.
Kuhusu ujio wa kocha mpya, Try Again amesema mchakato unaendelea vizuri na atapatikana siku chache zijazo ili aje ashiriki mwenyewe katika zoezi la usajili wakati msimu ukielekea ukingoni.
“Wanasimba msiwe na hofu, tumejipanga vilivyo kurudi kwenye ubora wetu. Tutafanya usajili mkubwa na Rais wa Heshima amenihakikishia yupo tayari kutoa fedha kufanikisha jambo hili.
“Mchakato wa kumpata kocha unaendelea vizuri nadhani ndani ya siku chache zijazo atakuwa amekuja tayari kwa kuanza usajili pamoja na maandalizi ya msimu (pre season),” amesema Try Again.