Kikosi chetu kimefanya mazoezi ya kwanza hapa Tunisia tayari kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CS Sfaxien utakaopigwa Jumapili Januari 5.
Mazoezi hayo yamefanyika katika Uwanja wa nje wa Olympique De R – Tunis ambao ndio utatumika kwa ajili ya mchezo wetu siku ya Jumapili saa moja usiku kwa saa za Tanzania.
Wachezaji wote 22 tuliosafiri nao kwa ajili ya mchezo huo wameshiriki mazoezi hayo kikamilifu na wapo kwenye hali nzuri huku wakiendelea kuzoea hali ya hewa.
Akizungumzia hali ya kikosi tangu tulivyowasili Tunisia jana jioni, Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu Ahmed Ally amesema kila kitu kinaendelea vizuri na hali ya hewa sio baridi kali na haitakuwa kikwazo siku ya mchezo.
“Leo tumeanza mazoezi kwa siku ya kwanza, tutaendelea kesho pamoja na Jumamosi kabla ya kushuka dimbani Jumapili.
“Maandalizi kwa ujumla yanaendelea vizuri na jambo la kushukuru baridi sio kali kama tulivyoenda Algeria kwahiyo tunaamini tutakuwa na nafasi nzuri ya kupata matokeo chanya,” amesema Ahmed.