Kikosi chetu leo kimefanya mazoezi ya mwisho katika uwanja Obedi Itani Chilume katika mji wa FrancisTown ambapo kutapigwa mchezo wetu wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United kesho saa mbili usiku.
Wachezaji wote 22 tuliosafiri nao wameshiriki mazoezi hayo kikamilifu na wapo tayari kwa ajili ya kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye mchezo wa kesho.
Mapema leo mchana wakati akiongea na vyombo vya habari kocha Mkuu Fadlu Davids amenukuliwa akisema kuwa malengo yetu ni kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye mechi zote mbili nyumbani na ugenini ingawa haitakuwa kazi rahisi.
Fadlu amesema pamoja na ukubwa wa Simba lakini Gaborone United ni timu imara hasa ikichangiwa kuwa inacheza nyumbani mbele ya mashabiki wake.
“Naiheshimu Gaborone United kwa sababu ni Mabingwa hapa Botswana kwahiyo tunategemea kupata upinzani mkubwa lakini tupo tayari kwa ushindani,” amesema Fadlu.