Kikosi chetu kimefanya mazoezi ya mwisho katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, kujiandaa na mchezo wa kesho wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad Casablanca utakaopigwa saa 10 jioni.
Kiungo mkabaji Sadio Kanoute ambaye alikuwa majeruhi na amekosa mechi kadhaa zilizopita amerejea na ameshiriki mazoezi hayo na yuko tayari kuipambania timu kesho.
Kama Kocha Roberto Oliviera ‘Robertinho’ na wasaidizi wake kama wataona inafaa watatumia kiungo huyo kwenye mchezo wa kesho kwa kuwa yuko tayari.
Wachezaji wetu wote wameshiriki kikamilifu mazoezi hayo isipokuwa mlinda mlango, Aishi Manula ambaye hayupo fiti asilimia 100 wengine wote morali ipo juu tayari kuhakikisha wanafanya kila linalowezekana kupata ushindi wa nyumbani kesho.
Ingawa tunafahamu mchezo utakuwa ngumu na tunaiheshimu Wydad kutokana na ukubwa wake na historia yake lakini tupo tayari kuwakabili na kuwapa furaha Wanasimba.