Kikosi chetu kimefanya mazoezi ya kwanza leo hapa Uturuki kwa awamu mbili asubuhi na jioni.
Mazoezi ya asubuhi yalikuwa mepesi kutokana na benchi la ufundi kuhitaji wachezaji kuweka miili sawa kwani siku mbili nyuma walikuwa kwenye safarini.
Kocha wa viungo, Corneille Hategekimana amesimamia mazoezi haya ambapo walianza kukimbia taratibu nusu uwanja kabla yakuanza ya viungo ikiwemo kutumia vifaa mbalimbali kama fimbo fupi za kuruka, koni na vinginevyo.
Mazoezi ya jioni yalikuwa ya nguvu ambapo makocha wote wanne kila mmoja alikuwa na eneo lake la kusimamia programu aliyoweka na muda mwingine walifanya kazi hiyo kwa pamoja.
Baada ya kumaliza mazoezi hayo mawili kocha mkuu, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ alitoa programu nyingine ya kucheza mpira aina tofauti na muda mwingi alikuwa akilenga kwenye eneo la ufundi huku yakisimamiwa na wasaidizi wake.
Kocha Robertinho amesema imekuwa bahati kwa upande wake kwakuwa amewakuta wachezaji wapo kwenye hali nzuri na utimamu sababu kila aina ya mazoezi aliyopanga wafanye wametimiza kwa ufanisi kitu ambacho amekifurahia.
“Tumeanza vizuri mazoezi, kadri siku zinavyozidi kwenda tutakuwa tunadilisha mbinu mbalimbali. Jambo zuri kwangu kuona wachezaji wote wanahamu ya kufanya kila ambacho nahitaji kutokea kwao,” amesema Robertinho.