Timu kuondoka kesho Alfajiri kuifuata Berkane

Kikosi chetu kitaondoka kesho saa 11 alfajiri kuelekea nchini Morocco tayari kwa mchezo wa kwanza wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane utakaopigwa Jumamosi, Mei 17.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu, Ahmed Ally kwa niaba ya Uongozi ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Saluhu Hassan kwa kutupa Ndege ambayo itatupeleka na kuturidisha kwa ajili ya kutufanya tuwe na utulivu kwenye maandalizi yetu.

Ahmed amesema kikosi kitaondoka Dar es Salaam na kutua moja kwa moja katika Jiji la Casablanca kabla ya kuelekea Berkane ambapo mchezo huo utapigwa huku wachezaji wakipata muda mwingi wa kufanya maandalizi kitu ambacho Simba inazidi kutoa shukrani za dhati kwa Serikali.

Ahmed ameongeza kuwa kuelekea mchezo huo tumekuja na kauli mbiu ambayo ni  ‘TUNABEBA’ tukiwa na maana kuwa tumejipanga kuhakikisha tunalibakisha taji la Kombe la Shirikisho Afrika.

Ahmed ameenda mbali zaidi na kuwaomba Wanasimba kuwa wamoja na kila mtu kwa nafasi yake ahakikishe anaiwezesha timu kuchukua taji la Kombe la Shirikisho msimu huu.

“Kama kila mtu alifanya jitihada hadi timu kufika hapa ilipo basi anatakiwa kuongeza jitihada hizo mara 100 ili kuhakikisha Simba itabakisha Kombe la Shirikisho katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.”

“Berkane ni timu bora na ina historia nzuri kwenye michuano hii lakini tumeapa kuwa hatutaki yajitokeze ya mwaka 1993 safari hii tunataka kubeba taji,” amesema Ahmed.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER