Timu ipo kamili Kuivaa Mashujaa Leo

Kikosi chetu leo saa 10 jioni kitashuka katika Uwanja wa KMC Complex kuikabili Mashujaa FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC ambao tunategemea utakuwa mgumu.

Tunarejea kwenye ligi baada ya kupita siku nyingi kutokana na ushiriki wetu kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ambayo tumeingia hatua ya fainali.

Pamoja na kufanikiwa kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika pia malengo yetu ya kupambana kuhakikisha tunatwaa ubingwa bado yapo hivyo kila mchezo kwetu ni muhimu kupata pointi tatu.

Mara zote tulizokutana na Mashujaa wamekuwa wakitupa upinzani mkubwa lakini hata hivyo tumejipanga vizuri kuwakabili na malengo yetu leo kupata pointi tatu.

Kutoka benchi la ufundi hichi ndicho walichosema…….

Kocha Msaidizi, Seleman Matola amesema Mashujaa ni timu nzuri na ina kocha bora mwenye uzoefu, Salum Mayanga lakini tumejiandaa kuhakikisha tunaweza kuwadhibiti.

Ligi inaelekea ukingoni na kila timu inahitaji kupata pointi tatu ili kuzidi kujiweka kwenye nafasi nzuri lakini sisi malengo yetu ni ubingwa hivyo kila mechi kwetu ni fainali.

“Tunategemea mchezo mgumu kutoka kwa Mashujaa lakini tumejiandaa na tupo tayari kupambana mpaka mwisho ili kupata pointi tatu,” amesema Matola.

Awesu afunguka kwa niaba ya wachezaji…..

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji kiungo mshambuliaji, Awesu Awesu amesema kila mchezo kwetu ni fainali na malengo yetu ni kupata pointi tatu.

“Tangu tumeanza msimu huu mechi zote tulizocheza ni ngumu na hata ya kesho itakuwa ngumu lakini tumejiandaa kuhakikisha tunashinda,” amesema Awesu.

Tuliwafunga Mzunguko wa Kwanza Lake Tanganyika…….

Katika mchezo uliopita wa mzunguko wa Kwanza uliopigwa uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma, Novemba Mosi, 2024 tuliibuka na ushindi wa bao moja.

Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji, Steven Mukwala kwa kichwa dakika ya mwisho akimalizia mpira wa kona uliopigwa na Awesu Awesu.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER