Kampuni ya SportPesa imeipa Klabu ya Simba fedha taslimu Sh 50,000,000 ikiwa ni bonasi baada ya kufanikiwa kufika hatua ya Robo Fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
SporPesa ndiyo wadhamini wakuu wetu na wameweka utaratibu wa kutoa bonasi kila timu inapofanya vizuri kwenye ligi ya ndani au michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mkurugenzi Mtendaji wa SportPesa, Tarimba Abbas ameipongeza timu yetu kwa kufika hatua hiyo na kukiri kuitendea haki hadhi ya kampuni hiyo kwa kuitangaza vizuri kimataifa.
Tarimba amesesema hii ni mara ya pili kwa timu yetu kufika hatua ya robo fainali kitu ambacho wao kama wadhamini wakuu wanajivunia kufanya kazi na sisi.
“Simba inazidi kuitendea haki ya brand yetu ya SportPesa, leo tumewakabidhi cheki ya Sh 50,000,000 ikiwa ni bonasi kwa kufanikiwa kufika Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kama ilivyo kwenye makubaliano ya mkataba wetu,” amesema Tarimba.
Naye Mtendaji Mkuu wa Klabu, Barbara Gonzalez amesema fedha hizo zitasaidia kwenye maandalizi ya timu kama safari, malazi na mambo mbalimbali ya kiundeshaji.
“Kwa niaba ya Klabu ya Simba, naipongeza SportPesa kwa hili jambo wanalofanya. Kiasi hiki wanachotoa kinatusaidia mambo mbalimbali ya kiundeshaji timu na tunajivunia kufanya nao kazi,” amesema Barbara.
Kwa niaba ya wachezaji mlinzi wa kushoto, Gadiel Michael ameishukuru SportPesa kwa kuendelea kutimiza makubaliano ya kimkataba na ameahidi msimu ujao tutafika hatua kubwa zaidi ya hii kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Kwa niaba ya wachezaji tunaishukuru SportPesa kwa kutimiza makubaliano ya mkataba na tunapenda kuwaahidi baada ya kujikwaa msimu ujao tutakuwa bora zaidi na kufika mbali kuliko tulivyofanya sasa,” amesema Gadiel.