Mchezo wetu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi Azam FC uliopigwa uwanja wa Azam Complex umemalizika kwa sare kufungana bao moja.
Mtanange huo ulianza kwa kasi huku tukishambuliana kwa zamu ingawa matumizi ya nguvu yalikuwa makubwa kipindi cha kwanza.
Azam walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 43 lililofungwa na Idd Seleman ‘Nado’ baada ya kupokea pasi ndefu iliyopigwa na Mudathir Yahya kutoka katikati mwa uwanja.
Kipindi cha pili tuliongeza kasi ya mashambulizi na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga ingawa hatukuweza kuzitumia vizuri.
Medie Kagere alitusawazishia bao hilo dakika ya 84 baada ya mpira mrefu uliopigwa na mlinzi David Kameta ‘Duchu’ kupanguliwa na mlinda mlango Wilbol Maseke kabla ya kumkuta mfungaji.
Kocha Didier Gomes aliwatoa Taddeo Lwanga, Said Ndemla na Hassan Dilunga na kuwaingiza Erasto Nyoni, Rally Bwalya na Chris Mugalu.
Tumebakisha mchezo mmoja dhidi ya Namungo utakaopigwa Uwanja Benjamin Mkapa, Julai 18 saa 10 jioni ambapo tutakabidhiwa taji letu la ubingwa hivyo tunawaomba mashabiki wetu kujitokeza kwa wingi kushuhudia sherehe hizo.