Mchezo wetu wa mwisho wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) dhidi ya Buyenzi kutoka Burundi uliopigwa Uwanja wa Abebe Bikila umemalizika kwa sare ya mabao 2-2.
PVP Buyenzi walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya pili kupitia kwa Rukiya Bizimana baada mpira uliopigwa kuokolewa na mlinda mlango Caroline Rufa kabla ya kumkuta mfungaji.
Jentrix Shikangwa alitupatia bao la kusawazisha dakika ya saba kwa shuti kali lilomshinda mlinda mlango wa PVP Adidja Nzeyimana baada ya kupokea pasi ndefu kutoka Kwa Ruth Ingosi.
Vivian Corazone alitupatia bao la pili dakika ya 18 baada kutumia vizuri makosa ya walinzi wa PVP na kuachia shuti kali lililomshinda mlinda mlango.
PVP walisawazisha bao hilo dakika ya 61 kufuatia mlinzi Daniela Ngoyi kujifunga wakati akijaribu kuokoa mpira wa kona uliopigwa na Channy Nsabiyumva.
Kocha Juma Mgunda alifanya mabadiliko ya kuwatoa Jentirx Shikangwa, Saiki Mary, Elizabeth Wambui, Violeth Nicholas na Precious Christopher na kuwaingiza Asha Rashid, Dotto Evarist, Amina Bilal, Jackline Albert na Asha Djafar.
Queens itakutana na Polisi Bullets kutoka Kenya katika mchezo wa Nusu Fainali ya michuano hiyo utakaopigwa Agosti 26.