Kikosi chetu leo kitatupa karata yake ya kwanza kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika Msimu wa 2021/22 kwa kucheza na Jwaneng Galaxy ya hapa Gabarone nchini Botswana.
Mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Taifa wa Botswana utaanza saa tisa kwa saa za hapa na kwa nyumbani ni saa 10 jioni.
Baada ya kufika nchini hapa jana alfajiri, wachezaji walipumzika na mchana walifanya mazoezi ya mwisho kuweka miili sawa kabla ya mtanange wa leo.
Maandalizi yamekamilika kwa asilimia 100 na wachezaji wote 24 waliosafiri wapo kwenye hali nzuri tayari kwa mchezo.
KAULI YA KOCHA GOMES
Kocha Mkuu Didier Gomes, amesema malengo yetu msimu huu ni kufika nusu fainali ya michuano hiyo hivyo inabidi kufanya vizuri kwenye mchezo wa leo ili mechi ya marudiano nyumbani iwe rahisi.
“Tunajua haitakuwa mechi rahisi, Galaxy ni timu nzuri na wanacheza soka la kushambulia lakini tuko tayari kuwakabili, tuliweza kuwatazama kupitia mkanda wa video kwahiyo tumejipanga,” amesema Gomes.
BOCCO ATOA NENO
Kwa upande wake Nahodha John Bocco, amesema wachezaji wote wapo tayari kwa ajili ya kuipambania bendera ya Simba na kila mmoja atakayepata nafasi atahakikisha anajitoa kwa asilimia zote ili kuleta ushindi.
TAARIFA YA KIKOSI
Katika mchezo wa leo tutakosa huduma ya nyota Jonas Mkude, Abdul Swamad Kassim na Ahmed Feruz ambao wamebaki jijini Dar es Salaam kusubiri mechi ya marudiano.
Mshambuliaji Chris Mugalu na kiungo Pape Ousmane Sakho wao hawakusafiri na kikosi kutokana na kuendelea kuuguza majeraha ingawa wako mbioni kurejea dimbani.
Nyota wengine Kibu Denis na Yusuf Mhilu pia wamebaki Dar es Salaam kutokana na kuchelewa kupata vibali kutoka Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), hivyo nao watacheza katika hatua inayofuata.