Kocha Mkuu, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema tumeutumia mchezo wa leo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Coastal Union kujiandaa na mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos ya Zambia.
Robertinho amesema katika mchezo wa leo amewatumia wachezaji wenye uzoefu ili kuzidi kutengeneza maelewano baina yao kuelekea mechi dhidi ya Power Dynamos itakayopigwa Oktoba Mosi.
Robertinho ameweka wazi kuwa amefurahishwa na jinsi wachezaji walivyocheza ingawa anaamini tulikuwa na nafasi ya kupata mabao mengi zaidi ya matatu tuliyofunga.
“Tumeutumia mchezo wa leo kujiandaa na mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos. Tulijua Coastal watatupa mechi ngumu ambayo itazidi kutuimarisha.
“Ukiangalia kikosi cha leo tumewatumia wachezaji wenye uzoefu ambao tunategemea kuwatumia dhidi ya Power Dynamos,” amesema Robertinho.
Akizungumzia ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Coastal, Robertinho amesema “tulikuwa na nafasi kubwa ya kupata mabao sita mpaka saba lakini matatu sio mbaya, nawapongeza wachezaji wangu.”