Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amechaguliwa kocha bora wa Ligi Kuu ya NBC wa mwezi Machi huku mshambuliaji Jean Baleke akichaguliwa mchezaji bora.
Robertinho ameshinda tuzo hiyo baada ya kuwapiku Nasreddine Al Nabi wa Yanga na Abdallah Mohamed ‘Baresi’ wa Tanzania Prisons ambao aliingia nao fainali.
Robertinho ametuongoza kupata ushindi mnono wa mabao 3-0 ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar katika mwezi Machi.
Kwa upande wa Baleke amewashinda Daruweshi Saliboko wa KMC na Jeremia Juma wa Tanzania Prisons ambao aliingia nao fainali ya kinyang’anyiro hicho.
Baleke amefunga mabao yote matatu ‘hat trick’ katika ushindi wa mabao 3-0 tuliopata ugenini dhidi ya Mtibwa.
Hii ni mara ya kwanza kwa Robertinho na Baleke kutwaa tuzo hiyo tangu wajiunge na kikosi chetu.
Tuzo hizo hutolewa kwa kocha na mchezaji ambao wamefanya vizuri kwa mwezi husika na huchaguliwa na Kamati Maalum kabla ya kutangazwa na Bodi ya Ligi.