Kocha Mkuu mesema siku zote anawaza vitu vikubwa na malengo yake ni makubwa ikiwemo kufika Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Robertinho ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili wa kuifundisha timu yetu amesema watu wengi wamekuwa wakifikiria kuhusu hatua ya makundi lakini ukiweka mipango mizuri hata fainali inawezekana.
Kuhusu ubingwa wa Ligi Kuu, Robertinho amesema yeye ni mshindani na anaamini katika mipango dhabiti hivyo kila kitu kinawezekana.
“Nimewahi kuwa mchezaji kabla ya kuwa kocha, siku zote naamini katika mipango mizuri. Ukiwa na mipango mizuri unaweza kufika nusu fainali mpaka fainali hilo linawezekana pia nikiwa hapa Simba.
“Wakati niko Vipers tulipokuwa tunaenda kukutana na TP Mazembe wengi waliamini ulikuwa mwisho wetu lakini tulikuwa na mipango mizuri mpaka tukafanikiwa kuwatoa,” amesema Robertinho.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Klabu, Murtaza Mangungu amesema kitu kilichotuvutia kwa Robertinho ni ubora na uzoefu wake kwa soka la Afrika Mashariki kwa hiyo tunaamini atatufikisha tunapopataka.
“Robertinho ni kocha mwenye wasifu mkubwa nasi tuna malengo makubwa ndiyo maana tumemchukua, ana uzoefu mkubwa wa soka la Afrika Mashariki hilo pia limetuvutia,” amesema Mangungu.