Timu yetu ya Wanawake ya Simba Queens imefanikiwa kutinga Fainali ya Michuano ya Ligi ya Mabingwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati CECAFA baada ya kuifunga AS Kigali WFC mabao 5-1 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Azam Complex.
Ushindi huo unatufanya kukutana na SHE Corporates kutoka Uganda katika mchezo wa fainali utakaopigwa Jumamosi uwanja wa Azam Complex.
Mchezo huo ulianza kwa kasi huku tukitawala sehemu kubwa huku tukifanya mashambulizi mengi langoni mwa AS Kigali lakini tulipoteza nafasi kadhaa za kufunga.
Kiungo mkabaji Aquino Corazone alitupatia bao la kwanza dakika ya 14 kabla ya Opa Clement kuongeza la pili dakika 30 ambapo dakika tisa baadaye Amina Ramadhani akongeza la tatu na kutufanya kwenda mapumziko tukiwa mbele kwa 3-1.
Kipindi cha pili tulirudi kwa kasi ile ile ambapo tuliongeza mengine mawili kupitia kwa Aquino dakika ya 47 na Diana William dakika ya 84.
Kocha Sebastian Nkoma aliwatoa Asha Djafari, Philomena Abakah na mlinda mlango Zubeda Mgunda na kuwaingiza Pambani Kuzoya, Olaiya Barakat na Gelwa Yona.
SHE Corporates tulikuwa nao kundi moja la B na tuliwafunga mabao 2-0 katika hatua ya makundi.