Simba Queens imefanikiwa kuibuka na ushindi wa bao moja dhidi ya Ceasiaa Queens katika mchezo wa mwisho wa Ligi ya Wanawake Serengeti Lite Women’s Premier League uliopigwa katika Uwanja wa Chuo Kikuu cha Mkwawa mkoani Iringa.
Tulianza mchezo huo kwa kasi huku tukitafuta bao la mapema ili kuwaweka wapinzani kwenye presha lakini tulishindwa kuzitumia nafasi tulizotengeneza.
Wenyeji Ceasiaa nao walikuja mara kadhaa langoni kwetu kutafuta bao lakini safu yetu ya ulinzi ilikuwa imara kuhakikisha hakuna jambo baya linalotukuta.
Kinara wa mabao Jentrix Shikangwa alitupatia bao la ushindi dakika ya 66 baada ya kumalizia mpira wa krosi uliopigwa na Joelle Bukuru.
Licha ya ushindi wa leo tumeshindwa kutetea ubingwa wetu baada ya wapinzani wetu JKT Queens kuwafunga Mkwawa Queens.