Simba Queens imefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Gets Program katika mchezo wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania (TWPL) uliopigwa Uwanja wa John Merlins jijini Dodoma.
Mchezo huo ulianza kwa kasi ya kawaida huku timu zikishambuliana kwa zamu lakini Queens walifika zaidi langoni mwa Gets na kumiliki sehemu kubwa ya mechi.
Jentrix Shikangwa alitupatia bao la kwanza dakika ya 11 kwa shuti kali nje ya 18 baada ya kumalizia pasi iliyopigwa na Asha Djafar.
Asha Djafar alitupatia bao la pili dakika ya 20 kwa kichwa akimalizia mpira wa krosi uliopigwa na Precious Christopher.
Baada ya mabao Queens iliendelea kumiliki sehemu kubwa ya mchezo huku ikitengeneza nafasi kadhaa ambazo kama tungekuwa makini tungeenda mapumziko tukiwa na mabao zaidi ya mawili tuliyofunga.
Kipindi cha pili tuliongeza tulirudi kwa kasi kuendelea kuliandama lango la Gets Program ambapo dakika ya 65 Shikangwa alitupatia bao la tatu kwa kichwa baada ya kumalizia mpira wa krosi uliopigwa na Wincate Kaari.
Kocha Yussif Basigi alifanya mabadiliko ya kuwatoa Aisha Mnunka, Precious Christopher, Violeth Nicholas, Ritticia Nabbosa Asha Djafar na kuwaingiza Jackline Albert, Janeth Nyagali, Shelda Boniface, Emeliana Mdimu na Zawadi Hamis
Matokeo haya yanatufanya kufikisha pointi 37 baada ya kucheza mechi 14.