Simba Queens kesho saa 10 jioni itashuka katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma kuikabili Fountain Gate kwenye mchezo wa Ligi ya Wanawake ya Serengeti Lite Women’s Premier League (SLWPL).
Leo kikosi cha Queens kimefanya mazoezi ya mwisho katika Uwanja wa Jamhuri na wachezaji wote wameshiriki.
Meneja wa timu, Seleman Makanya amesema kikosi kipo kwenye hali nzuri, morali ya wachezaji ipo juu na wapo tayari kupambana kuhakikisha tunapata ushindi.
Makanya ameongeza kuwa mchezo utakuwa mgumu kutokana na ubora walionao Fountain lakini tumejipanga kuhakikisha tunapata pointi zote tatu.
“Kikosi kipo kwenye hali nzuri, morali za wachezaji zipo juu tayari kwa mchezo wa kesho. Tunajua mchezo utakuwa mgumu lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda,” amesema Makanya.
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, Queens iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.